Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imeidhinisha rasmi marekebisho ya katiba ya Simba Sports Club baada ya kukamilika kwa mchakato wa kisheria chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo.
Uidhinishaji huo unaipa Simba mwanga wa kuanza utekelezaji wa katiba mpya inayolenga kuimarisha utawala bora, kuongeza uwajibikaji na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji katika klabu hiyo kongwe nchini.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, imewekwa bayana kuwa Simba Sports Club Company Limited ndiyo chombo kitakachosimamia masuala ya kibiashara na kiutendaji ya klabu. Hatua hiyo inalenga kutenganisha majukumu ya kiutawala na yale ya kibiashara kwa lengo la kuongeza ufanisi na ushindani katika soka la kisasa.
Aidha, umiliki wa hisa utaendelea kubaki chini ya Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama wa klabu, hatua inayolenga kulinda misingi ya umiliki wa wanachama na kuhakikisha maslahi yao yanabaki salama. Katiba hiyo pia imeainisha kuwa Baraza la Wadhamini litakuwa na wajumbe kati ya watano hadi saba, huku Mkutano Mkuu ukiendelea kuwa chombo chenye mamlaka ya mwisho ya maamuzi.
Akizungumza kuhusu uidhinishaji huo, Msajili wa Vyama vya Michezo, Abel Mathias Ngilungwa, amesema marekebisho hayo yamezingatia taratibu zote za kisheria na hayana athari kwa usalama wala hayachochei migogoro miongoni mwa wanachama.
Amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuimarisha misingi ya utawala bora, kulinda umiliki wa klabu na kuweka mazingira yatakayovutia uwekezaji zaidi, hatua inayotarajiwa kusaidia maendeleo ya Simba ndani na nje ya uwanja.
Wanachama na mashabiki wa Simba wametakiwa kuheshimu uamuzi huo na kushirikiana katika utekelezaji wa katiba mpya kwa manufaa ya klabu. Wadau wa michezo wanaamini kuwa mageuzi hayo yanaweza kuwa chachu ya mafanikio mapya kwa Simba katika mashindano ya ndani na kimataifa.



