Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cosmopolitan katika mchezo wa hatua ya 32 bora kombe la CRDB, ni matokeo muhimu kwao kwani wamekata tiketi ya kufuzu hatua ya 32 bora.
Kamwe amesema lengo lao kwenye mchezo huo ilikuwa ushindi na kusonga mbele bila ya kujali idadi ya mabao waliyofunga.
Kamwe ametoa kauli hiyo kuwajibu wale waliobeza ushindi huo wakiamini Yanga ilipaswa kufunga mabao mengi dhidi ya timu hiyo inayoshiriki ligi ya Championship.
Msemaji huyo wa mabingwa wa nchi amesema Yanga imetoka kucheza mechi ngumu za ligi ya mabingwa na pia wakikabiliwa na mfululizo wa mechi hivyo ilikuwa muhimu kwa benchi la ufundi na wachezaji kuchukua tahadhari.
"Nimeona maoni ya watu wengi walitaka tufunge mabao mengi, huo sio mpira wa miguu. Tumetoka kwenye mechi ngumu Jumapili, tumerudi Jumatatu kwa maana yake tumefanya mazoezi siku moja tu na kwa asilimia kubwa wamecheza wale wale waliotumika Jumapili."
"Hizi ni mechi za kurefresh, cha muhimu unapata matokeo unakwenda kwenye hatua inayofuata. Tuna mechi nyingine, Jumapili dhidi ya Namungo kule Ruangwa lakini pia tutakuwa na mechi tarehe 25 dhidi ya JKT hapa KMC Complex."
"Kwahiyo ni lazima wachezaji wetu wacheze kwa umakini mkubwa ili pia kujiepusha na majeraha na ndio maana wamecheza kwa tempo ya kawaida," alisema Kamwe