Inaelezwa beki wa kati wa Simba Abdulrazack Hamza atakuwa nje kwa muda mrefu ambapo nyota huyo huenda akawa ameumaliza msimu.
Hamza alipata jeraha katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Septemba 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Stadium, ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0. Tangu wakati huo, beki huyo hajarejea uwanjani.
Baada ya tathmini ya kitabibu, mchezaji huyo alipelekwa nchini Morocco kwa matibabu zaidi katika Kliniki ya Zerktouni ambako alifanyiwa upasuaji Desemba Mosi mwaka jana. Awali kulikuwa na matumaini kuwa angeweza kurejea mapema katika mzunguko wa pili wa ligi, lakini hali imekuwa tofauti.
Chanzo cha ndani ya klabu kimebainisha kuwa ingawa maendeleo yake ni mazuri, madaktari wamependekeza apate muda mrefu zaidi wa mapumziko na uangalizi maalum ili kuhakikisha anapona kikamilifu kabla ya kurejea dimbani.
“Kwa sasa anaendelea vizuri, lakini taratibu za kitabibu zinaonyesha hatarudi uwanjani hadi msimu uishe. Jeraha lilikuwa kubwa kuliko ilivyodhaniwa mwanzo,” kilieleza chanzo hicho.
Msimu huu Simba imekabiliwa na changamoto katika safu yake ya ulinzi kwani wakati wakimkosa Hamza, pia Wekundu hao wa Msimbazi wanamkosa Wilson Nangu aliyefanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu Afrika Kusini jana.
Nangu aliumia kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Esperance uliopigwa dimba la Mkapa na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kwa sasa eneo hilo linawategemea zaidi nahodha msaidizi Rushine de Reuck na Ismail Toure aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo.