Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Barker amesema wamekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa na mchezo huo wakitua mkoani Dodoma jana ambapo leo watakuwa na nafasi ya kukamilisha maandalizi yao.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema anatambua hakuna mechi nyepesi kwenye ligi kuu ya NBC hivyo hawatawadharau wapinzani wao.
"Sisi tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons hapo kesho. Maandalizi yetu yanakwenda vyema na kwa takribani miezi miwili niliyokuwa hapa tumekuwa na maandalizi ya kimbinu na uchezaji wetu"
"Jana baada ya safari ndefu tulifanya mazoezi ytu ya kwanza hapa na leo tutakamilisha maandalizi yetu."
"Natambua hakuna mechi nyepesi, tunafahamu wapinzani watatupa upinzani wa kutosha licha ya kuwa hawako kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi. Tumefanya maandalizi mazuri ya kimbinu na kiakili ili wachezaji wangu waende kufanya vizuri kwenye mchezo huu," alisema Barker
Wekundu hao wa Msimbazi wataikabili Tanzania Prisons kesho Jumapili katika mchezo utakaopigwa saa 3 usiku.