Real Madrid yaweka rehani uongozi La Liga baada ya kipigo

Joel JJ By Joel JJ • 22nd February 2026


Real Madrid yaweka rehani uongozi La Liga baada ya kipigo

Klabu ya Real Madrid imejikuta katika wakati mgumu kwenye mbio za ubingwa wa La Liga baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya CA Osasuna usiku wa Jumamosi, Februari 21, 2026.

Mchezo huo uliochezwa katika dimba la El Sadar Stadium ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia dakika za mwanzo, huku wenyeji wakionyesha dhamira ya kusaka ushindi mbele ya mashabiki wao.

Osasuna walipata bao la kwanza dakika ya 38 kwa njia ya penalti iliyofungwa na mshambuliaji wao Ante Budimir. Penalti hiyo ilitolewa baada ya mwamuzi kujiridhisha kupitia VAR kufuatia tukio tata ndani ya eneo la hatari la Madrid.

Real Madrid walirudi kwa nguvu kipindi cha pili na kusawazisha dakika ya 73 kupitia nyota wao wa kibrazil Vinicius Junior, aliyemalizia vizuri pasi ya haraka kutoka kiungo wa kati. Bao hilo lilirejesha matumaini kwa wageni na kuamsha presha kwa wenyeji.

Hata hivyo, matumaini ya Madrid yalizimwa katika dakika za nyongeza baada ya Raúl García kufunga bao la ushindi, bao lililothibitishwa baada ya ukaguzi mwingine wa VAR. Filimbi ya mwisho ilikuta Osasuna wakishangilia ushindi muhimu huku Madrid wakiondoka wakiwa wameinama.

Kwa matokeo hayo, Real Madrid wanabaki kileleni kwa pointi 60, lakini sasa uongozi wao uko hatarini. FC Barcelona, waliopo nafasi ya pili, wanashuka dimbani leo dhidi ya Levante UD.

Endapo Barcelona watashinda mchezo huo, watapanda kileleni mwa msimamo na kuipiku Madrid, hali itakayoongeza joto katika mbio za ubingwa wakati msimu ukiingia hatua za mwisho.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.