Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC juzi ulikuwa na maana kubwa kwa Wananchi.
Ukiacha thamani ya alama hizo tatu walizopata ugenini, ambazo ziliwapandsha nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tatu dhidi ya vinara wa ligi hiyo JKT Tanzania, ushindi huo unawaweka karibu na rekodi nyingine ya kutopoteza mchezo kwa muda mrefu kwenye ligi kuu.
Mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mchezo kwenye ligi kuu ya NBC ni Novemba 07 2024 ikichapwa mabao 3-1 na Tabora United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Azam Complex.
Tangu wakati huo, Yanga haijapoteza tena mechi ya ligi kuu kwa takribani miezi 15 wakicheza mechi 29.
Kama Wananchi hawatapoteza mchezo unaofuata dhidi ya JKT Tanzania basi watafikisha mechi 30 bila ya kupoteza mchezo ambapo ni sawa na kucheza msimu mzima.



