Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kiwango walichoonyesha kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji jana ambao ulimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliopigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, Barker alisema wachezaji wake walicheza kwa kujitoa sana lakini kilichokosekana ni alama tatu tu.
"Nawapongeza wachezaji wangu kwa kile walichoonyesha leo (jana). Tumecheza mechi ngumu sana lakini nimeridhishwa na jinsi timu ilivyocheza."
"Tumecheza kwa kujitolea sana, nafikiri kuna vitu vichache vya kuongeza ili tuwe bora zaidi. Kama tutaendelea kucheza hivi, tutashinda mechi nyingi," alisema Barker
Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Yanga ambao utapigwa Jumapili March 1 uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Barker alisema wanakwenda kufanya maandalizi sahihi kuelekea mchezo huo wa dabi ya Kariakoo.
Barker amesema kikosi chake kitaelekea Zanzibar mapema ili kwenda kukamilisha maandalizi hayo akileta kushinda mchezo huo.
"Mechi dhidi ya Yanga tutajiandaa kama tunavyojiandaa kwenye mechi nyingine, tutahakikisha tunajiandaa vizuri. Tutafanya recovery na kisha kuelekea Zanzibar mapema iwezekanavyo."
"Hii ni dabi kubwa hivyo tutahakikisha tunajiandaa ili tuweze kupata alama tatu," alisema Barker



