Ligi Kuu ya NBC imeendelea leo ambapo mechi mbili zilipigwa mkoani Singida na Mwanza.
Wenyeji Singida Black Stars walitumia vyema uwanja wa nyumbani wakiichapa Coastal Union bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Airtel.
Bao pekee la ushindi kwa Singida BS lilifungwa na mshambuliaji Joseph Guede.

Mkoani Mwanza Azam Fc imenusurika na kichapo mbele ya Pamba Jiji wakilazimisha sare ya mabao 2-2.
Pamba Jiji ilijipatia bao la kwanza dakika ya 45 kupitia kwa kiungo wa Azam, Himid Mao, aliyejifunga (OG) wakati akijaribu kuokoa shambulizi. Mapema kipindi cha pili, dakika ya 48, John Ben Nakibinge aliipatia Pamba bao la pili na kuifanya Azam ionekane kuelekea kupoteza mchezo huo.
Hata hivyo, mabadiliko ya mbinu ya kocha Florent Ibenge yalizaa matunda haraka. Ndani ya dakika tatu za maajabu, Azam walirudi mchezoni: Dakika ya 56: Jean Jaques Ngita aliifungia Azam bao la kwanza. Dakika ya 59: Kiungo fundi, Feisal Salum 'Fei Toto', alisawazisha kwa mkwaju wa penalti.
Hata hivyo Feisal hakumaliza mchezo huo akitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi mlinzi wa Pamba Jiji Abdulmajid Mangalu.
Feisal anatarajiwa kukosa mechi mbili lakini ni wazi atauwahi mchezo wa dabi dhidi ya Yanga utakaopigwa March 15
Matokeo haya yameleta mabadiliko kidogo kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Pamba Jiji FC imefikisha pointi 24 baada ya kucheza mechi 15, wakisalia katika nafasi ya nne.
Azam FC: Wamefikisha pointi 23 katika michezo 11, wakishika nafasi ya tano huku wakiwa na faida ya michezo minne mkononi dhidi ya Pamba.



