Jana Azam Fc ilishindwa kuondoka na alama zote tatu mkoani Mbeya baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Wakati Kocha wa Tanzania Prisons Shadrack Nsajigwa akifurahia alama hiyo moja, Florent Ibenge wa Azam Fc amelalamika timu yake kukosa matokeo kwa sababu ya ubovu wa uwanja wa Sokoine.
"Ni ngumu kupata ushindi katika mazingira kama haya. Huu sio uwanja wa kucheza mpira wa miguu. Unapocheza katika uwanja kama huu hakuna ufundi, wachezaji wanalazimika kupiga tu mpira".
"Sio kama tunalalamika, tunazungumza uhalisi na jambo muhimu kwetu tumeweza kuondoka na alama moja kwa hiyo tunakwenda kujiandaa na mechi nyingine zinazofuata," alisema Ibenge.
Huo ulikuwa mchezo wa pili mfululizo Azam Fc inakosa ushindi ugenini baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo uliopita.
Wauza Ice cream hao wamepanda nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakifikisha alama 24 lakini wakiwa wamecheza mechi moja zaidi ya Simba inayoshika nafasi ya nne pia ikiwa na alama 24