Mikiki mikiki ya ligi kuuya NBC inaendelea leo kwa mechi za viporo kupigwa katika viwanja mbalimbali.
Timu ya TRA United itakuwa mwenyeji wa Namungo Fc katika mchezo wa mapema utakaopigwa saa nane mchana katika uwanja wa Black Rhino Arusha.
Majira ya saa 10:15 jioni mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini kati Singida BS dhidi ya Simba utapigwa uwanja wa Airtel Mtipa huku Singida.
Hii ni mechi inayowakutanisha miamba wawili ambao wote walikuwa na majukumu ya michuano ya Kimataifa msimu huu Simba ikicheza ligi ya mabingwa na Singida BS kombe la Shirikisho.
Timu hizo zimekuwa na ushindani wa aina yake kila zinapokutana ambapo mara ya mwisho Singida BS waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa nusu fainali kombe la CRDB msimu uliopita.
Saa 1:15 usiku, Dodoma Jiji watahitimisha mechi za leo kwa mchezo dhidi ya Azam Fc uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Azam Fc wamekosa ushindi katika mechi mbili zilizopita pengine leo watashuka uwanjani wakiwa na dhamira ya kuondoka na alama zote tatu.
Hata hivyo wanakutana na Dodoma Jiji ambayo msimu huu imejipambanua kwa kutopoteza mchezo kwenye uwanja wake wa nyumbani.