Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo ambapo michezo miwili inatarajiwa kupigwa katika viwanja tofauti.
Mchezo wa mapema saa 10, Mbeya City itaikaribisha Singida BS katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.
Mchezo huo utafuatiwa na mechi kubwa inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, dabi ya Dar es salaam kati ya Azam Fc dhidi ya Yanga utakaopigwa saa 2:30 usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Unapozungumzia dabi, Azam Fc na Yanga pengine ndio dabi yenye ushindani zaidi pengine kuliko hata ile ya Kariakoo kwa kuangalia matokeo ya mechi za karibuni.
Msimu uliopita Azam Fc walishinda mchezo mmoja na Yanga pia wakashinda mchezo mmoja huku kila timu ikifunga mabao mawili katika mechi hizo mbili.
Msimu huu ni Azam Fc na Yanga pekee ambazo hazijapoteza mchezo kwenye ligi mpaka sasa.
Yanga ndio vinara wa ligi wakikusanya alama 35 baada ya mechi 13 wakati Azam Fc wakishika nafasi ya tatu wakikusanya alama 27 baada ya mechi 13 pia.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi mwezi Januari mwaka huu Yanga ikiibuka mabingwa kwa mikwaju ya penati baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Ni wazi zitakuwa dakika 90 ngumu kwa kila upande lakini zenye burudani ya aina yake kwa mashabiki wa soka nchini.
