Mchezo wa ligi kuu ya NBC kati ya Azam Fc dhidi ya Yanga uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, umemalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Ni mchezo uliotawaliwa na ufundi mwingi lakini nafasi chache zikitengenezwa na kila upande pengine kutokana umakini uliokuwa eneo la ulinzi kwa timu zote.
Azam Fc ilianza mchezo huo kwa kasi na mapema tu walimpa kazi mlinda lango wa Yanga Djigui Diarra kuokoa hatari langoni.
Hata hivyo kipindi cha pili ni Yanga iliyokuwa bora zaidi ikitawala mchezo kwa muda mwingi lakini uimara wa Azam Fc kuanzia eneo la kiungo liliwapa wakati mgumu washambuliaji wa Yanga kupenya.
Dakika za lala salama mshambuliaji Prince Dube aliangushwa ndani ya eneo la hatari lakini mwamuzi wa mchezo huo 'akapotezea' tukio hilo ambalo pengine lingeipa Yanga nafasi ya kufunga.
Ni alama moja kwa kila timu Yanga ikiendelea kusalia kileleni na alama 36 huku Azam Fc wakisogea nafasi ya pili wakifikisha alama 28.



