Kocha Mkuu wa Young Africans Sports Club, Pedro Gonçalves, amewapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha ujasiri mkubwa na kutokubali kushindwa hata katika nyakati ngumu.
Kauli hiyo ameitoa muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya TRA United, uliomalizika kwa sare ya bila kufungana. Licha ya matokeo hayo kutokidhi matarajio, kocha huyo alisisitiza kuwa timu yake imeonyesha uthabiti wa hali ya juu.
Mchezo huo ulikuwa wa kukamilisha mechi 15 za duru ya kwanza ya ligi, ambapo Yanga imefanikiwa kumaliza ikiwa kileleni mwa msimamo. .
Akizungumza baada ya mchezo, Gonçalves alisema:
“Nusu ya kwanza ya msimu imekamilika na tuko nafasi ya kwanza. Ingawa matokeo ya leo si yale tuliyotarajia, tunaondoka na uhakika mkubwa kwamba uimara wetu ni wa chuma. Nataka kupongeza ujasiri na kujitolea kwa wachezaji wetu, ambao wameendelea kupambana licha ya changamoto nyingi na majeraha.”
Aliongeza kuwa wakati wanaanza safari hiyo, walikuwa nyuma ya wapinzani wao, lakini sasa wanaongoza ligi kutokana na juhudi na mshikamano wao.
“Tulipoanza changamoto hii, tulikuwa nyuma ya wapinzani wetu. Leo tunaangalia msimamo na kuona matunda ya kazi yetu ngumu — sisi ni vinara wa wazi. Tupo kileleni kwa juhudi zetu wenyewe, na hapo ndipo tunapokusudia kubaki.”
Kocha huyo alihitimisha kwa kueleza fahari yake kwa kikosi hicho, akisisitiza kuwa timu inaendelea kusonga mbele kwa pamoja huku ikijiandaa na changamoto zinazofuata.



