Yanga yamrejesha Moalin kumsaidia Goncalves

Joel JJ By Joel JJ โ€ข 23rd March 2026


Yanga yamrejesha Moalin kumsaidia Goncalves

Uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kumrejesha kocha Abdihamid Moalin kuwa Kocha Msaidizi huku Pedro Goncalves akiendelea na majukumu yake ya Kocha Mkuu.

Taarifa iliyotolewa na Yanga baada ya kikao kirefu kati ya uongozi na benchi la ufundi kujadili changamoto zilizojitokeza kwenye duru ya kwanza, hatua hiyo imefikiwa baada ya uongozi kubaini kuwepo kwa changamoto ya kiufundi ambayo imepelekea timu isicheze kwa mfumo uliozoeleka.

Moalin alifanya kazi na makocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi msimu uliopita, Yanga ikiamini urejeo wake unakwenda kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi.

Hii hapa sehemu ya taarifa iliyotolewa na Yanga;

TAARIFA KWA UMMA

MACHI 23, 2026

Uongozi wa Young Africans Sports Club, leo tarehe 23-03-2026 umekutana Makao Makuu ya Klabu, Jangwani Jijini Dar Es Salaam na kufanya kikao cha tathimini ya timu yetu (Menโ€™s Senior Team), baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

Kikao kilianza kwa Uongozi kupokea ripoti ya kikosi chetu kutoka kwa Benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Pedro Soares Goncalves ambapo ripoti hiyo ilionyesha baadhi ya takwimu nzuri za timu katika mzunguko wa kwanza.

Mpaka sasa, Young Africans Sports Club tumecheza michezo 16, tukishinda michezo kumi na moja (11), sare tano (5) na hatujafungwa mchezo wowote ule.

Vile vile, Young Africans Sports Club ndio timu iliyofunga magoli mengi zaidi kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, magoli 32 huku tukiwa na rekodi nzuri pia ya kuruhusu magoli machache kuliko timu nyingine, magoli matatu tu.

Hata hivyo, baada ya kuipitia kwa kina ripoti hiyo ya benchi la ufundi, Uongozi umebaini changamoto kadhaa zilizoisumbua timu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi:

1. Ratiba

Ndani ya siku 21, Kikosi chetu kimecheza michezo 7 mfululizo, michezo 6 ya Ligi Kuu na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho la CRDB. Ratiba hii pia ilijumlisha na safari ya umbali wa Kilomita 4,462 kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mechi za ugenini. Uongozi unaamini safari hizi na ratiba kubana kulipunguza ufanisi wa wachezaji kutokana na uchovu uliopatikana.

2. Majeraha

Mpaka sasa, timu yetu ina wachezaji 8 muhimu ambao wamepata majeraha tofauti tofauti yaliyowapelekea kukosa michezo. Khomein Aboubakar, Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka, Edmund John, Prince Dube na Laurindo Maria "Depu". Wachezaji watatu kwenye orodha hii wamepata majeraha yatakayowaweka nje mpaka mwisho wa msimu.

Aidha, licha ya changamoto hizo, Uongozi umegundua uwepo wa changamoto ya kiufundi inayoifanya Timu icheze aina tofauti ya uchezaji (style of play), na ile ambayo imezoeleka na kuendana na wachezaji walio ndani ya kikosi.

Changamoto hii ya kiufundi imekuwa sababu ya kuifanya timu kupata wakati mgumu kupata matokeo mazuri na kucheza vizuri pia kwenye baadhi ya michezo ya Ligi Kuu.

Uamuzi wa Uongozi

Hivyo, katika kuitatua changamoto hii, Uongozi wa Young Africans Sports Club umefikia uamuzi wa kumuongeza kwenye benchi la Ufundi, Kocha Abdihamid Moalin kama Kocha Msaidizi wa Kocha Pedro Goncalves.

Kocha Moalin amewahi kuhudumu katika Klabu yetu kama Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Msaidizi katika vipindi tofauti chini ya Kocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi na kupata mafanikio makubwa ya kushinda Kombe la Ligi Kuu 2024/2025, Kombe la Shirikisho la CRDB 2025 na Kombe la Muungano 2025. Uongozi wa Young Africans SC unamkaribisha Kocha Moalin na kumtakia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya kwa kushirikiana na Makocha wengine ndani ya kikosi chetu.

Mwisho, Uongozi wa Young Africans unapenda kuwaahidi Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Klabu yetu kuwa, Timu yetu itarudi mzunguko wa pili ikiwa Imara na nguvu kubwa kuelekea kutimiza malengo yetu kwa Msimu wa 2025/26, kwa kushinda Ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na Kombe la Shirikisho la CRDB.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.