Kocha wa zamani wa Liverpool FC, Jürgen Klopp, amekanusha vikali tetesi zinazomuhusisha na kujiunga na Real Madrid, akisisitiza kuwa hapakuwahi kuwa na mawasiliano yoyote kati yake na klabu hiyo.
“Habari zote zinazosambaa ni uzushi mtupu,” alisema Klopp. “Hawajawahi kunipigia hata mara moja, wala wakala wangu hajawahi kupigiwa simu. Kwa utani, ningependa hata kuichukua Atlético Madrid kwa wakati mmoja. Samahani Madrid, mtalazimika kupiga simu kwanza.”
Kocha huyo wa zamani wa Liverpool pia alifunguka kuhusu maisha yake baada ya kuachana na ukocha, akieleza kuwa kwa sasa amejitenga kabisa na masuala ya soka na anafurahia maisha ya kawaida nje ya uwanja.
“Tangu niondoke Liverpool, hata sikuwa najua ni lini mechi zinachezwa; nilikuwa nimejitenga kabisa,” alisema. “Nimekuwa nikifanya mazoezi, kufurahia maisha, na kutumia muda mwingi na wajukuu wangu… mambo ya kawaida kabisa, nikiwa najua sitarejea kufanya kazi ya ukocha.”
Klopp aliongeza kuwa kwa sasa hana mpango wowote wa kurejea kwenye benchi la ufundi, akibainisha kuwa hana hisia ya kukosa ukocha licha ya uzoefu wake mkubwa katika mchezo huo.
“Sasa nina miaka 58. Kama ningeanza tena ukocha nikiwa na miaka 65, watu wangekumbusha kuwa niliwahi kusema sitarejea. Ningeweza kuwaambia kuwa nilimaanisha kwa dhati wakati huo,” alieleza. “Lakini kwa kweli, sijisikii kama kuna kitu ninachokikosa kwa kutokuwa kocha.”