Kocha wa Coventry City, Frank Lampard, yuko mbioni kuweka historia mpya ndani ya klabu hiyo, huku wito ukizidi kuongezeka kuhusu uwezekano wa kurejea kwake katika katika klabu ya Chelsea.
Lampard alichukua mikoba ya kuinoa Coventry mwaka 2024 wakati timu hiyo ikiwa kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini tangu wakati huo ameiongoza katika mabadiliko makubwa na ya kushangaza. Chini ya uongozi wake, Coventry imepanda hadi nafasi za mtoano wa kupanda daraja, kufika kileleni mwa msimamo wa EFL Championship, na kuweka tofauti ya pointi tisa dhidi ya wapinzani wao.
Aidha, timu hiyo imeonyesha makali makubwa katika safu ya ushambuliaji, ikiwa imefunga mabao 81 na kuwa na safu bora zaidi ya ushambuliaji katika ligi hiyo. Kwa sasa, ushindi katika michezo mitatu ijayo unaweza kuwahakikishia ubingwa na kurejea katika Premier League kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.
Mafanikio hayo hayajapita bila kutambuliwa, ambapo Nicky Butt ameibuka hadharani kumuunga mkono Lampard kurejea Chelsea. Butt anaamini klabu hiyo inapaswa kuwaamini tena mastaa wake wa zamani na kumpa Lampard nafasi ya kuinoa timu hiyo kabla ya kumalizika kwa msimu huu.
Wakati Coventry ikiwa karibu kufikia mafanikio makubwa ya kupanda daraja, na sauti zenye ushawishi zikiongezeka zikimtaka kurejea Stamford Bridge, kurejea kwa makali kwa Lampard kunazidi kuwa moja ya simulizi zinazovutia zaidi katika ulimwengu wa soka kwa sasa.
Lampard balaa jipya mjini.



