Senegal yawasilisha rufaa CAS kupinga kuvuliwa ubingwa Afcon 2025

Joel JJ By Joel JJ • 25th March 2026


Senegal yawasilisha rufaa CAS kupinga kuvuliwa ubingwa Afcon 2025

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limewasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliowavua ubingwa wa Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya CAF uliotolewa Machi 17, 2026, uliobatilisha ushindi wa Senegal dhidi ya Morocco katika fainali na kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0, kwa madai kuwa Senegal walikiuka kanuni za mashindano.

Senegal walikuwa wametangazwa mabingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika fainali iliyochezwa jijini Rabat, lakini mchezo huo ulitawaliwa na utata wa maamuzi ya marefa uliosababisha wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani kwa muda wakipinga uamuzi wa penalti waliodai haukuwa halali.

Katika rufaa yao, FSF imeeleza kuwa uamuzi wa CAF haukuwa wa haki na haukuzingatia mazingira halisi ya tukio hilo. Shirikisho hilo linataka matokeo ya awali yaheshimiwe na Senegal irejeshewe ubingwa wao.

“Tunapinga kwa nguvu zote uamuzi huu ambao unaonekana kuwa wa upendeleo na usiozingatia sheria za mchezo,” ilieleza sehemu ya taarifa ya FSF.

Kwa upande wake, CAF imesisitiza kuwa ilifuata kanuni zilizopo, ikieleza kuwa kitendo cha timu kutoka uwanjani kinachukuliwa kama kujitoa, jambo linalostahili adhabu kwa mujibu wa taratibu za mashindano.

Mahakama ya CAS tayari imepokea rufaa hiyo na inatarajiwa kupanga ratiba ya kusikiliza kesi hiyo katika wiki zijazo.

Sakata hilo limeibua mjadala mkubwa barani Afrika, huku wachambuzi wa soka wakieleza kuwa linaweza kuwa na athari kwa taswira na uaminifu wa mashindano ya AFCON iwapo halitashughulikiwa kwa haki na uwazi.

Uamuzi wa CAS utakuwa wa mwisho na wa kisheria katika mzozo huo unaovuta hisia za mashabiki wa soka kote barani Afrika.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.