Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepata pigo baada ya kufungwa bao 1-0 na Liechtenstein katika mchezo wa FIFA Series uliopigwa jana, Machi 26, 2026, katika Uwanja wa Kigali PelΓ©.
Bao pekee la mchezo lilifungwa na mshambuliaji wa Liechtenstein, Ferhat Salam, katika dakika ya 56, akitumia vyema uzembe wa safu ya ulinzi ya Tanzania.
Katika kipindi cha kwanza, timu zote zilicheza kwa tahadhari huku zikishambuliana kwa zamu bila mafanikio ya kupata bao. Tanzania ilionekana kumiliki mpira kwa muda mwingi, lakini ilikosa umakini katika eneo la mwisho.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, lakini ni Liechtenstein walioweza kutumia nafasi yao ya kwanza muhimu kufunga bao la ushindi. Baada ya bao hilo, Tanzania iliongeza mashambulizi na kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Kocha wa Taifa Stars Miguel Gamondi alilazimika kufanya mabadiliko ya kiufundi ili kuimarisha safu ya ushambuliaji, lakini safu ya ulinzi ya Liechtenstein ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho.
Matokeo hayo ni ya kushtua kwa Tanzania, ikizingatiwa kuwa Liechtenstein ni miongoni mwa timu zenye rekodi dhaifu katika soka la kimataifa. Hata hivyo, ushindi huo ni muhimu kwa Liechtenstein katika mashindano haya ya FIFA Series yanayolenga kuzipa timu kutoka mabara mbalimbali uzoefu wa ushindani.
Kwa upande wa Tanzania, kipigo hicho kinatoa funzo muhimu kuhusu umuhimu wa kutumia nafasi za kufunga na kuimarisha safu ya ulinzi kabla ya mechi zijazo.
Taifa Stars wanatarajiwa kurejea uwanjani March 29 kucheza dhidi ya Macau kuhitimisha mechi ya pili ya FIFA Series.