Azam Fc yaipeleka dabi ya Mzizima Azam Complex

Joel JJ By Joel JJ β€’ 28th March 2026


Azam Fc yaipeleka dabi ya Mzizima Azam Complex

Mchezo wa ligi kuu ya NBC kati ya Azam Fc dhidi ya Simba maarufu Mzizima Derby ambao umepangwa kupigwa Jumapili ya Apri 05, 2026, utapigwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Azam Fc ambao ndio wenyeji wa mchezo huo, wamechagua kutumia uwanja wao wa nyumbani, Azam Complex na sio uwanja wa Benjamin Mkapa kama ilivyozoeleka.

Awali kulikuwa na tetesi kuwa mchezo huo ungepigwa 'Lupaso' kama ilivyozoeleka lakini licha ya Serikali kuridhia matumizi ya dimba la Mkapa kwenye baadhi ya mechi, wauza Ice Cream hao wamechagua kupeleka mechi Chamazi dhamira yao ikiwa kuzisaka alama tatu zaidi kuliko mapato.

Mechi ya duru ya kwanza iliyopigwa Disemba 07 2025 Simba wakiwa wenyeji, ilipigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na Azam Fc kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wakati huu timu hizo zinakutana tena kila moja ikihitaji alama tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye mbio za ligi kuu.

Azam FC na Simba zinatofautiana alama mbili tu kwenye msimamo wa ligi, Simba ikiwa nafasi ya pili na alama 31 wakati Azam Fc wako nafasi ya tatu wakiwa na alama 29.

Hata hivyo Azam Fc wamecheza mechi moja zaidi ya Simba hivyo kuwa na uhitaji wa kushinda mchezo huo ili kupunguza gap la pointi dhidi ya wapinzani wao hao.

Azam Fc inayonolewa na kocha Florent Ibenge, msimu huu imeimarika zaidi ikimaliza mechi 15 za duru ya kwanza bila ya kupoteza.

Ni Azam Fc na Yanga pekee ambazo hazijapoteza mchezo wa ligi kuu msimu huu. Hata hivyo wanakwenda kukutana na Simba iliyoimarika zaidi baada ya maboresho waliyofanya kwenye usajili wa dirisha dogo.

Ujio wa kocha Steve Barker na usajili wa wachezaji kama Ismael Toure, Libasse Gueye, Anicet Oura, Inno Loemba na Clatous Chama umeiongezea Simba makali.

Baada ya kulikosa taji la ligi kuu kwa misimu minne mfululizo, Wekundu hao wa Msimbazi msimu huu wamepania kushinda taji hilo ambalo kwa muda wote huo limeishi kwenye makabati ya watani zao wa jadi, klabu ya Yanga.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.