Shirika la soka la Afrika CAF limefunga mjadala unaohusu ubingwa wa AFCON 2025 kwa kuwa suala hilo limepangwa kusikilizwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo, Misri, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, Patrice Motsepe, alisema CAF haizungumza tena kuhusu tukio hilo, bali itaelekeza nguvu zake katika kuheshimu taratibu za kisheria zinazoshughulikia kesi hiyo.
"Mechi ya fainali kati ya Senegal na Morocco, si jambo muhimu sana kwetu kuendelea kulijadili…” alisema Motsepe, akibainisha kuwa CAF inathamini hisia kubwa zinazohusiana na mpira wa miguu lakini sasa ni muhimu kusubiri uamuzi wa CAS.
Motsepe amesema Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ambayo ndiye chombo cha juu zaidi kushughulikia mashindano na migogoro ya kimichezo duniani, na kwamba shirikisho hilo litaenzi na kutekeleza uamuzi wowote utakaochukuliwa na mahakama hiyo.
"Suala hili tayari liko mbele ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS)… na sisi tutaheshimu na kutekeleza uamuzi wowote utakaochukuliwa,” alisema Motsepe, akiweka wazi msimamo wa CAF wa kufuata utaratibu wa kisheria.
Sakata hili lilizuka mwezi Machi wakati CAF ilipopiga marufuku matokeo ya mechi ya fainali ya AFCON 2025, na kubadilisha ushindi wa Senegal kuwa ushindi wa 3–0 kwa Morocco, kufuatia kitendo cha Senegal kuondoka uwanjani kwa muda kupinga uamuzi wa mwamuzi kuhusu penalti.
Uamuzi huo ulizua hasira na kushinikiza Shirika la Soka Senegal kufungua kesi mbele ya CAS, likidai uamuzi wa CAF haukufuata taratibu za kisheria.
Katika hatua isiyo ya kawaida, Senegal ilionyesha kombe la AFCON katika mchezo wa kirafiki jijini Paris, licha ya kunyimwa rasmi ubingwa, ikionyesha msimamo wao wa kudai taji hilo.
Hadi sasa, CAS imepokea rasmi rufaa ya Shirikisho la Soka la Senegal na inaendelea kusikiliza hoja za pande zote mbili kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho juu ya ubingwa wa AFCON 2025.
Kwa upande wake, CAF imekuwa ikiwekeza jitihada za kuimarisha uaminifu na sheria ndani ya mashindano yake, huku Motsepe akisisitiza kuwa baraza la nidhamu na kamati za rufaa za CAF zinaundwa na wanasheria na majaji wenye heshima barani Afrika.



