Meneja wa habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kikosi cha Yanga leo Jumatatu kinaingia kambini kuanza maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Jumamosi, April 04 katika uwanja wa KMC Complex.
Kamwe amesema Yanga inarejea mazoezini ikiwa na nyota wote ambao hawakuhusika na majukumu ya timu za Taifa katika kalenda ya FIFA.
"Timu inaingia kambini Jumatatu (leo) kuanza maandalizi ya mchezo wetu unaofuata kwa mujibu wa ratiba ambao ni dhidi ya Tanzania Prisons."
"Mchezo huo utapigwa uwanja wa KMC Comples siku ya Jumamosi, April 04 saa 12:30 jioni."
"Baada ya mapumziko tunatarajia wachezaji wetu wote ambao hawakuwa na majukumu ya timu za Taifa na wale ambao hawana changamoto za majeruhi, wataingia kambini na ari kubwa kujiandaa na mchezo huo," alisema Kamwe.
Akizungumzia taarifa ya wachezaji majeruhi, Kamwe amesema mshambuliaji Prince Dube, beki Ibrahim Bacca, Chadrack Boka na Edmund John wanatarajiwa kuungana na wenzao kwenye mazoezi wakianza na mazoezi ya Gym.
Kamwe amesema mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' bado anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa daktari na pengine anaweza kuanza mazoezi baada ya wiki moja.
Aidha Kamwe amethibitisha wachezaji Dickson Job na Clement Mzize wameondolewa kwenye mipango ya timu kwa mechi zilizobaki msimu huu kutokana na hali zao baada ya kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini.



