Jana mashabiki wa soka nchini kwa mara nyingine walimshuhudia Ahmed Arajiga, refa wa kimataifa kutoka Tanzania, akipeperusha bendera ya Tanzania kwa ustadi wa hali ya juu, akiongoza mechi ya kuwania mshindi wa tatu wa Kundi A la FIFA Serie kati ya Kenya na Grenada kwenye Uwanja wa Amahoro, Rwanda.
Mechi hiyo ilikuwa tamasha la soka, na Kenya ikionyesha nguvu zao kwa ushindi wa 3-0. Mabao yakifungwa na Austine Odhiambo, Ryan Ogam na Vijay Valcin akijifunga na kuihakikishia Kenya ushindi huo.
Kwa Arajiga, hii ilikuwa ni moja ya mechi muhimu sana baada ya muda mrefu, kwani mara yake ya mwisho uwanjani ilikuwa Januari 29, 2026, kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC ambapo Simba SC ilishinda 2-0 dhidi ya Mashujaa FC. Lakini ujuzi wake wa kimataifa umezidi kuimarika, akionyesha kwamba Tanzania ina refa wa kiwango cha juu, anayefahamika na wachezaji, timu, na mashabiki.
Arajiga hakucheza peke yake, alisaidiwa na wenzake watanzania Mohamed Mkono na Respicous Dismas, huku Nassir Siyah akihudumu kama refa wa akiba. Ushirikiano huu wa unaonesha jinsi Tanzania inavyoanza kuchomoza kwa kutoa waamuzi ngazi za kimataifa.
