Chama cha Soka cha Ghana (GFA) kimeanza mazungumzo na kocha wa zamani wa Morocco Walid Regragui, kuhusu uwezekano wa kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo, maarufu kama Black Stars.
Taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari barani Afrika zinaeleza kuwa Regragui ni miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kushika wadhifa huo, huku mazungumzo kati yake na GFA yakiwa tayari yameanza, ingawa bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa.
Hatua hiyo ya GFA inakuja kufuatia mabadiliko ya benchi la ufundi baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Otto Addo hali iliyochangiwa na matokeo yasiyoridhisha katika mechi za hivi karibuni za kimataifa.
Walid Regragui anatajwa kuwa chaguo bora kutokana na rekodi yake nzuri, hasa baada ya kuiongoza Morocco kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, mafanikio yaliyoweka historia kwa bara la Afrika.
Hata hivyo, kocha huyo aliondoka hivi karibuni kuinoa Morocco kufuatia changamoto zilizojitokeza baada ya mashindano ya Africa Cup of Nations 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ushindani wa nafasi hiyo ni mkubwa huku makocha wengi kutoka ndani na nje ya Afrika wakitajwa kuwania kibarua hicho.
Endapo Walid Regragui atateuliwa, anatarajiwa kupewa jukumu la kuiandaa GhanaΒ kwa mashindano yajayo ya kimataifa ikiwemo FIFA World Cup 2026.
Hadi sasa, GFA haijatoa tamko rasmi kuhusu uteuzi wa kocha mpya.