Sakata la usajili wa kiungo wa Yanga, Mohamed Damaro Camara, limechukua sura mpya baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulitupilia mbali rasmi shauri lililowasilishwa na klabu ya Simba SC.
Kupitia taarifa iliyotolewa Aprili 2, 2026 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, kamati hiyo imebainisha kuwa haina sababu za kuendelea na shauri hilo baada ya kubaini kuwa usajili wa mchezaji huyo uko halali na haukiuki kanuni zilizotajwa.
Simba walikuwa wamefungua malalamiko wakidai kuwa usajili wa Damaro unaifanya Yanga kuwa na idadi ya wachezaji wa kigeni 13, kinyume na kanuni zinazoruhusu wachezaji 12 pekee kwa kila timu ya Ligi Kuu.
Aidha, klabu hiyo ilieleza kuwa usajili huo unakiuka Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu pamoja na taratibu za usajili zilizoainishwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Katika uamuzi wake, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeeleza wazi kuwa hoja zilizowasilishwa na Simba hazina msingi wa kisheria kwa mujibu wa kanuni husika, na kwamba mchezaji huyo habanwi na masharti yaliyotajwa katika malalamiko hayo.
Hivyo, kwa mujibu wa kamati hiyo, usajili wa Mohamed Damaro Camara uko sahihi na unakidhi vigezo vyote vya kikanuni.



