Kipaji cha soka kutoka Tanzania, Barka Seif Mpanda, kimeandika historia mpya baada ya kujiunga na akademi maarufu ya FC Barcelona, La Masia, kwa mkataba wa miaka mitano.
Barka anakuwa Mtanzania wa kwanza kujiunga na akademi hiyo inayotambulika duniani kwa kuzalisha nyota wakubwa wa soka akiwemo Lionel Messi, Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Sergio Busquets.
Mshambuliaji huyo mwenye kipaji kikubwa ametokea katika akademi ya CD Damm nchini Hispania, ambako alionyesha kiwango cha juu kilichowavutia mabingwa hao wa La Liga.
Katika msimu wake wa mwisho akiwa CD Damm, Barka alifunga mabao 41 katika mechi 28, takwimu zilizomfanya kuwa mmoja wa vijana waliokuwa wakifuatiliwa kwa karibu na vigogo mbalimbali wa soka nchini humo.
Kusajiliwa kwake na Barcelona ni matokeo ya maendeleo makubwa aliyoyaonyesha katika miaka ya hivi karibuni, huku uwezo wake wa kufunga mabao, kasi, ubunifu na uelewa wa mchezo vikitajwa kuwa baadhi ya sifa zilizowashawishi viongozi wa La Masia kumpa nafasi.
Hatua hiyo ni mafanikio makubwa si kwa Barka pekee bali pia kwa soka la Tanzania, kwani inafungua ukurasa mpya kwa vijana wengine wenye ndoto za kucheza katika akademi na vilabu vikubwa duniani.
Kwa kujiunga na La Masia, Barka atapata mazingira bora ya maendeleo ya kisoka pamoja na fursa ya kujifunza falsafa ya mchezo inayotumiwa na FC Barcelona tangu ngazi za vijana hadi timu ya kwanza.





