Canada imeandika historia katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibamiza Qatar mabao 6-0 katika mechi ya Kundi B iliyochezwa mjini Vancouver. Ushindi huo ni wa kwanza kabisa kwa Canada katika historia ya michuano ya Kombe la Dunia kwa wanaume.
Nyota wa Canada, Jonathan David, alikuwa gumzo la usiku huo baada ya kufunga mabao matatu (hat-trick) na kuiongoza timu yake kupata ushindi mkubwa wa kihistoria. Mabao mengine yalifungwa na Cyle Larin pamoja na Nathan Saliba huku Qatar pia ikijifunga bao moja.
Mchezo huo uligeuka kuwa mgumu zaidi kwa Qatar baada ya wachezaji wake wawili kuonyeshwa kadi nyekundu, hali iliyowapa Canada nafasi ya kutawala mchezo kuanzia kipindi cha kwanza hadi mwisho. Ushindi huo umeifanya Canada kupanda kileleni mwa Kundi B na kuongeza matumaini ya kutinga hatua ya mtoano.
Hata hivyo, furaha ya Canada iligubikwa na majeraha mabaya ya kiungo IsmaΓ«l KonΓ© aliyelazimika kutolewa nje kwa machela baada ya kuumia vibaya mguuni. Tukio hilo lilisababisha taharuki kubwa uwanjani na hata kuzua mvutano kati ya wachezaji wa timu zote mbili baada ya mechi.
Mbali na ushindi wa Canada dhidi ya Qatar, michezo mingine imetoa matokeo yafuatayo:
Czechia 1-1 South Africa
Switzerland 4-1 Bosnia and Herzegovina
Mexico 1-0 South Korea
Matokeo hayo yameifanya Mexico kujiimarisha katika Kundi A ikiongoza kundi huku Switzerland nayo ikituma salamu kali kwa wapinzani wake katika Kundi B.



