Klabu ya Simba SC imefikia makubaliano ya pande mbili na kiungo mshambuliaji Joshua Mutale maarufu kama Budo ya kuvunja mkataba wake, hatua inayomfanya nyota huyo kuwa mchezaji huru kuanzia sasa.
Taarifa zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya Mutale kumaliza kipindi chake cha mkopo katika klabu ya Al Adalah FC ya Saudi Arabia, huku timu hiyo ikiiarifu Simba kuwa haina mpango wa kumnunua moja kwa moja.
Mutale alikuwa bado amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Simba, lakini kutokana na makubaliano hayo mapya, pande zote zimeamua kuhitimisha ushirikiano wao mapema na kumpa nafasi mchezaji huyo kuanza safari mpya ya soka akiwa huru kuchagua hatma yake.
Kiungo huyo alitua Simba SC kwa matarajio makubwa kutokana na kiwango alichokuwa amekionyesha kabla ya kusajiliwa, lakini alishindwa kuonesha makali yaliyotarajiwa ndani ya kikosi hicho katika kipindi chake cha kuitumikia klabu hiyo.
Baada ya kipindi chake cha mkopo kumalizika nchini Saudi Arabia, Mutale sasa anatajwa kurejea katika mazingira aliyoyazoea baada ya kuhusishwa na klabu yake ya zamani ya Power Dynamos, timu ambayo Simba ilimsajili kutoka huko misimu miwili iliyopita.



