Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Julián Álvarez, ameripotiwa kuongeza shinikizo la kutaka kuondoka Atlético Madrid ili kutimiza ndoto yake ya kujiunga na Barcelona, katika sakata linaloendelea kuvuta hisia kubwa kwenye soka la Ulaya.
Kwa mujibu wa taarifa, Álvarez ameonesha nia ya wazi ya kuangalia changamoto mpya ya kikazi, hali iliyoendelea kuibua maswali kuhusu hatma yake ndani ya klabu ya Atlético Madrid.
Barcelona ilituma ofa ya kwanza ya kumsajili nyota huyo wa Argentina inayokadiriwa kufikia euro 100M, lakini ikakataliwa kabla ya Real Madrid kuwasilisha ofa ya euro 150M ambayo nayo ilikataliwa.
Atlético Madrid wameweka msimamo mkali kuhusu mchezaji huyo, wakisisitiza kuwa hawana mpango wa kuuza kirahisi. Klabu hiyo inadaiwa kumwekea mkataba wa muda mrefu unaoendelea hadi 2030 pamoja na kipengele cha kuvunja mkataba kinachofikia takribani euro milioni 500.
Viongozi wa Atlético wanaamini kuwa Álvarez bado ni sehemu muhimu ya mipango yao ya muda mrefu, hivyo hawako tayari kupokea ofa isiyokidhi thamani ya mchezaji huyo.
Hata hivyo baada ya Alvarez mwenyewe kuweka hadharani matamanio yake ya kujiunga na Barcelona, hatua hiyo huenda ikafungua mlango mwingine wa majadiliano baina ya Barcelona na Atletico Madrid na pengine mwafaka kufikiwa siku za usoni.
Kwa sasa Alvarez yuko na kikosi cha Argentina kwenye michuano ya kombe la Dunia nchini Marekani.



