Mtibwa Sugar leo wataikaribisha Simba SC katika mchezo muhimu wa NBC Premier League huku kila timu ikiwa na jambo kubwa la kupigania. Wenyeji Mtibwa wanatafuta pointi za kujinasua katika hatari ya kushuka daraja, wakati Simba wakisaka ushindi wa kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa.
Mchezo huo unakuja wakati ambapo Mtibwa Sugar wanakabiliwa na presha kubwa ya matokeo kutokana na nafasi yao kwenye msimamo wa ligi. Kila alama imekuwa ya thamani kwa timu hiyo ya Morogoro ambayo inahitaji kumaliza msimu katika nafasi salama ili kuendelea kubaki kwenye ligi kuu msimu ujao.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Afisa Habari na Mawasiliano wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema timu yao ipo tayari kupambana kwa nguvu zote dhidi ya Simba. "Tutapambana kwa nguvu kubwa sana, tuharibu mipango ya Simba leo ili tupate alama tatu zituweke mahali pazuri. Na sisi tunataka kusema kwenye ligi tumetibua mipango ya Simba msimu huu ya kutwaa ubingwa," alisema Kifaru.
Kwa upande wa Simba, ushindi leo ni muhimu katika harakati zao za kuwania ubingwa. Wekundu hao wa Msimbazi wanaingia uwanjani wakijua kuwa wanahitaji pointi tatu ili kuendelea kumkaribia vinara wa ligi Yanga, ambao kwa sasa wanaongoza kwa tofauti ya alama mbili.
Mbali na mchezo wa Morogoro, macho ya Simba na mashabiki wao yatakuwa pia Zanzibar ambako Yanga wanakabiliwa na mtihani mgumu dhidi ya Azam FC. Matokeo ya mchezo huo yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika sura ya mbio za ubingwa huku Simba wakitarajia Azam kuwazuia watani wao.
Hata hivyo, kabla ya kuangalia kitakachotokea Zanzibar, Simba watalazimika kwanza kuimaliza kazi yao dhidi ya Mtibwa Sugar. Kwa kauli ya Kifaru na hali ya Mtibwa ya kupambana dhidi ya kushuka daraja, mchezo wa leo una kila sababu ya kuwa mmoja wa mechi ngumu na zenye ushindani mkubwa katika hatua hii ya mwisho ya msimu.



