Timu ya taifa ya Morocco imeendelea kuonyesha ubora wa soka la Afrika katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kufuzu hatua ya 32 bora kufuatia ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Haiti katika mchezo wa mwisho wa Kundi C.
Katika mechi iliyochezwa jijini Atlanta, Morocco ililazimika kupambana kwa nguvu baada ya kujikuta ikipata wakati mgumu mbele ya na Haiti katika kipindi cha kwanza ikienda mapumziko na sare ya mabao 2-2.
Haiti ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza mapema kupitia bao lililoandikwa kama la kujifunga la kipa Yassine Bounou, kabla ya nahodha Achraf Hakimi kusawazisha dakika ya 39. Hata hivyo, Wilson Isidor aliirejesha Haiti mbele kwa shuti kali, lakini Ismael Saibari akaisawazishia Morocco kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa huku Haiti ikionyesha kiwango kizuri licha ya kuwa tayari ilikuwa imeondolewa mashindanoni. Morocco iliongeza presha na hatimaye kupata bao la tatu kupitia mfungaji mahiri Soufiane Rahimi dakika ya 78 kabla ya kinda Gessime Yassine kufunga bao la nne dakika ya 89 na kuhitimisha ushindi huo muhimu.
Ushindi huo umeifanya Morocco kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi C ikiwa na pointi saba, idadi sawa na Brazil iliyomaliza kileleni kutokana na ubora wa tofauti ya mabao. Atlas Lions sasa imefuzu rasmi hatua ya 32 bora na itaumana na mshindi wa Kundi F katika mechi ya mtoano.
Morocco imekuwa moja ya timu zinazovutia katika mashindano haya baada ya kuanza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Brazil na kufuatiwa na ushindi wa 1-0 dhidi ya Scotland kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao manne dhidi ya Haiti.
Matokeo hayo yanaifanya kuwa moja ya timu zinazobeba matumaini ya bara la Afrika katika mbio za kutwaa taji la dunia.
Baada ya mchezo huo, kocha Mohamed Ouahbi alikiri kuwa kikosi chake kilipata wakati mgumu dhidi ya Haiti lakini akasisitiza kuwa jambo muhimu zaidi lilikuwa kupata ushindi na kufuzu hatua inayofuata.
Kwa upande mwingine, Haiti, licha ya kumaliza bila pointi, ilipongezwa kwa kupambana kwa moyo mkubwa na kufunga mabao yake ya kwanza katika Kombe la Dunia tangu kushiriki kwao mwaka 1974.



