Kaimu Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Yahya Abushehe, amesema siku chache zilizobaki za NBC Premier League zitakuwa na majibu ya maswali mengi yanayowasumbua mashabiki wa soka nchini, ikiwemo nani atatwaa ubingwa, nani atasalia ligi kuu na nani atashuka daraja.
Abushehe ametoa kauli hiyo baada ya kupongeza namna mechi zote nane za mzunguko uliopita zilivyochezwa kwa wakati mmoja na kuoneshwa mubashara kupitia Azam TV, jambo alilosema limeongeza ushindani na kuwapa mashabiki fursa ya kufuatilia kila kinachoendelea katika mbio za ubingwa na vita ya kushuka daraja.
Ameeleza kuwa macho ya wengi sasa yataelekezwa kwenye michezo ya Juni 27 na Juni 30, ambapo hatima ya msimu wa 2025/26 itaamuliwa. Swali kubwa likiwa ni kama bingwa atapatikana mapema Juni 27 au kama ushindani utaendelea hadi mchezo wa mwisho wa msimu.
Mbali na mbio za ubingwa, Abushehe amesema vita ya kusalia ligi kuu nayo imezidi kupamba moto huku baadhi ya timu zikihitaji matokeo mazuri ili kuepuka kushuka daraja au kucheza mechi za mtoano.
"Majibu yote yatapatikana katika siku hizi za mwisho za msimu. Mashabiki waendelee kufuatilia kwa sababu kila mchezo una umuhimu mkubwa," amesema Abushehe.
Kwa sasa, mashabiki wa soka Tanzania wanasubiri kwa hamu kuona nani atakayetwaa taji la NBC Premier League na ni timu zipi zitakazofanikiwa kutimiza malengo yao kabla ya pazia la msimu kushushwa rasmi.



