Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) imeandika historia mpya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Uzbekistan na kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026.
DR Congo ilijikuta nyuma mapema kufuatia bao la Uzbekistan, lakini ilionyesha moyo wa kupambana na kurejea kwa nguvu katika kipindi cha pili. Yoane Wissa alisawazisha kwa mkwaju wa penalti kabla ya mshambuliaji Fiston Mayele kufunga bao la pili lililowapa Leopards uongozi na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wao.
Wissa alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika za nyongeza.
Kwa Mayele, hili lilikuwa bao lake la kwanza katika fainali za Kombe la Dunia, akiendelea kuthibitisha ubora wake kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.
Ushindi huo umeiwezesha DR Congo kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yake ya ushiriki wa Kombe la Dunia, ikiwa ni miaka 52 tangu iliposhiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1974 ikiwa inajulikana kama Zaire. Katika hatua ya 32 bora, DR Congo itavaana na England katika pambano litakalokuwa na ushindani mkubwa.
Historia imeandikwa, na sasa macho ya Waafrika wengi yataelekezwa kwa Leopards wakisaka kuendelea kufanya maajabu kwenye Kombe la Dunia 2026.
Hatua ya 32 bora DR Congo watachuana na Uingereza



