Timu ya Taifa ya Uingereza imeonyesha ubora wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Panama katika mchezo wa mwisho wa Kundi L na kutinga hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 ikiwa kinara wa kundi.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Uingereza ilirejea kwa kasi kipindi cha pili ambapo Jude Bellingham alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 62 kwa shuti kali lililoivunja ngome ya Panama. Dakika tano baadaye, nahodha Harry Kane alifunga bao la pili kwa kichwa akimalizia pasi ya Bellingham na kuhitimisha ushindi muhimu wa Three Lions.
Bao hilo lilikuwa la 11 kwa Kane katika historia ya Kombe la Dunia, likimfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Uingereza katika michuano hiyo baada ya kumpita Gary Lineker. Wakati huo huo, Bellingham aliendelea kung'ara kwa kufunga bao moja na kutoa asisti moja katika mechi hiyo.
Ushindi huo umeifanya Uingereza kumaliza kileleni mwa Kundi L ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na Croatia, huku Ghana ikifuzu kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu. Panama ilimaliza mkiani mwa kundi na kuaga mashindano bila kufuzu hatua ya mtoano.
Katika hatua ya 32 bora, Uingereza itakutana na DR Congo, timu iliyomaliza nafasi ya pili katika Kundi K baada ya ushindi wake wa mabao 3-1 dhidi ya Uzbekistan. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku England ikisaka kuendeleza safari yake ya kutwaa taji la dunia kwa mara ya pili katika historia yake.



