Mzunguko wa mwisho wa NBC Premier League msimu wa 2025/26 utakaochezwa apo kesho unatarajiwa kutoa hatma ya Timu za Fountain Gate, Mbeya City, Mtibwa, na Tanzania Prison ambazo zinapambana kujikwamua kushuka daraja .
Jedwali la ligi linaonyesha ushindani mkubwa kati ya timu hizo nne. Fountain Gate wanashika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 30, huku Mbeya City na Tanzania Prisons wakifuatia katika nafasi ya 13 na 14 kila moja ikiwa na pointi 29, zikitenganishwa na tofauti ya mabao. Mtibwa Sugar wako nafasi ya 15 wakiwa na pointi 27, hali inayowaweka katika mazingira magumu zaidi kuelekea mzunguko wa mwisho wa msimu. Tofauti ndogo ya pointi inaifanya kila matokeo ya kesho kuwa na uzito mkubwa katika kuamua hatma ya kila timu.
Mechi za mwisho zitachezwa kwa wakati mmoja, jambo litakaloongeza ushindani kutokana na kila timu kutolijua matokeo ya wapinzani wao moja kwa moja. Mtibwa Sugar watahitaji ushindi ili kuongeza nafasi ya kubaki ligi kuu, huku Mbeya City na Tanzania Prisons zikihitaji kupata matokeo mazuri pamoja na kutegemea yatakayopatikana katika viwanja vingine. Kwa upande wa Fountain Gate, pointi 30 walizonazo zinawapa nafuu ndogo, lakini bado hawajajihakikishia usalama ikiwa watapoteza mchezo wao wa mwisho huku wapinzani wao wakipata ushindi.
Mbeya City, ambao walirejea NBC Premier League msimu huu baada ya kupanda kutoka Championship, sasa wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kuhakikisha hawarudi tena . Tanzania Prisons, timu yenye historia ndefu ya kupambana na changamoto za kushuka daraja, nayo ipo kwenye presha kubwa ya kuendelea kusalia ligi kuu. Kwa Mtibwa Sugar, klabu yenye historia ya mafanikio katika soka la Tanzania, msimu huu umekuwa mgumu na sasa inalazimika kupigania uhai wake hadi dakika za mwisho. Fountain Gate nayo itahitaji kutumia vyema nafasi ya mwisho kuhakikisha inamaliza msimu ikiwa salama.
Historia ya Ligi Kuu Tanzania imewahi kushuhudia timu zikibadili hatma yao katika mzunguko wa mwisho wa msimu, ambapo ushindi au sare moja umeamua nani anabaki na nani anaondoka. Hali hiyo inatarajiwa kujirudia tena Juni 30, huku ushindani ukiwa mkali kutokana na tofauti ndogo ya pointi kati ya timu zinazopigania kuendelea kubaki kwenye ligi.
Filimbi ya mwisho ya mechi za kesho haitahitimisha tu msimu wa NBC Premier League 2025/26, bali pia itaweka wazi majina ya timu zitakazoshuka daraja na zitakazolazimika kucheza mechi za mtoano. Mwisho wa siku, ni timu zitakazotumia vizuri dakika 90 za mwisho ndizo zitakazoendelea kubaki kwenye ligi kuu, huku nyingine zikilazimika kuanza maandalizi ya safari mpya nje ya ligi ya juu ya soka nchini.



