Klabu ya Simba SC imefikia hatua za mwisho za kumsajili kiungo wa kimataifa wa Nigeria Ibraheem Jabaar kutoka Stellenbosch FC ya Afrika Kusini.
Taarifa zinaeleza kuwa makubaliano ya awali kati ya Simba SC na mchezaji huyo yamekamilika na anatarajiwa kuwasili Tanzania kwa ajili ya kukamilisha usajili wake rasmi.
Vyanzo kutoka ndani ya uongozi wa Simba, vimedokeza kuwa Jabaar ameandaliwa mkataba wa miaka miwili ambao utamuweka katika klabu hiyo hadi mwaka 2028 iwapo kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.
Usajili huu umefanyika kufuatia mapendekezo ya kocha Steve Barker ambaye anafahamu vyema uwezo wa mchezaji huyo kutokana na kufanya naye kazi hapo awali.
Barker anaamini Jabaar anaweza kuongeza ubora katika safu ya kiungo ya Simba kuelekea msimu wa 2026/27 kutokana na uelewa wake wa mfumo wa uchezaji.
Jabaar mwenye umri wa miaka 23 ameondoka Stellenbosch akiwa mchezaji huru baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya. Akiwa klabuni hapo amecheza zaidi ya mechi 140, akifunga mabao sita na kutoa pasi saba za mabao.
Ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati, kiungo mshambuliaji na winga wa kushoto, hali inayompa kocha chaguo zaidi katika safu ya ushambuliaji.



