Real Madrid wametoa taarifa rasmi kukanusha uvumi uliokuwa ukisambaa kuhusu madai ya kutaka kumsajili kiungo wa Chelsea, Enzo Fernández. Klabu hiyo imesisitiza kuwa haijawahi kufanya mawasiliano yoyote, ya moja kwa moja wala yasiyo ya moja kwa moja, kwa ajili ya kumsajili nyota huyo wa Argentina.
Katika taarifa hiyo, Real Madrid imeeleza wazi kuwa haina mpango wowote wa kuwasilisha ofa kwa Enzo Fernández, huku ikisisitiza kuwa taarifa zilizosambazwa katika siku za karibuni hazina ukweli wowote.
Mabingwa hao wa Hispania pia walimpongeza Enzo kwa ubora wake mkubwa uwanjani, wakimtaja kuwa ni mchezaji mwenye kiwango cha juu, lakini wakabainisha kuwa hilo halimaanishi wana nia ya kumsajili.
Aidha, Real Madrid imeonyesha heshima kubwa kwa Chelsea, ikieleza kuwa ina uhusiano mzuri wa kiutawala na klabu hiyo na kwamba misingi ya uaminifu na heshima baina ya taasisi hizo ndiyo sababu iliyowafanya kutoa ufafanuzi huo rasmi.
Mwisho, Real Madrid imeeleza kusikitishwa na kuendelea kusambazwa kwa taarifa zisizo sahihi ambazo zinasababisha mkanganyiko kwa mashabiki na kuathiri taswira ya klabu pamoja na watu wanaohusika, ikisisitiza kuwa uvumi wote unaowahusisha na usajili wa Enzo Fernández hauna msingi wowote.



