Klabu ya Yanga SC imetozwa faini ya Shilingi milioni 100 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufuatia kutotumia chumba rasmi cha kuvulia katika mchezo wa NBC Premier League dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, wachezaji na benchi la ufundi la Yanga walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja badala ya chumba rasmi cha kuvulia, kitendo kilichokiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mechi.
Mbali na faini hiyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imewapeleka kwa Kamati ya Maadili ya TFF Rais wa Yanga, Hersi Said, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, kwa tuhuma za kutoa maelezo yasiyo na msingi kuhusu tukio hilo.
Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi kifupi kwa Yanga kuchukuliwa hatua kwa kosa kama hilo, baada ya mwezi Mei 2026 pia kutozwa faini ya Shilingi milioni 30 kwa kukiuka utaratibu huo.
TAARIFA YA KAMATI
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Julai 2, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 233: JKT Tanzania FC 0-3 Young Africans SC
Klabu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh. 100,000,000 (milioni mia moja) kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kutokutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.
TAARIFA Katika hatua nyingine Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imewapeleka kwenye kamati ya Maadili ya TFF Rais wa Young Africans Hersi Said na Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo Andre Mtine ili kutoa maelezo ya msingi kutokana na makosa ya kujirudia ya uvunjifu wa kanuni inayoitaka timu kutumia vyumba rasmi vya kuvalia kwenye uwanja wa mchezo husika.
Klabu ya Young Africans mwezi Mei, 2026 ilitozwa faini ya Sh. 30,000,000 (milioni thelathini) kwa kosa mfanano na hili la kutotumia vyumba rasmi vya kuvalia kwenye uwanja wa mchezo na badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja.
Mechi Namba 234: Simba SC 1-0 KMC FC Klabu ya KMC imepewa onyo kali kwa kosa la wachezaji wake watatu (3) Aimari Said Twalibu jezi namba 71, Steven Donald Mgimwa jezi namba 80, na Hussein Ally Kihiyo jezi namba 86, kuvaa jezi zenye namba inayozidi sabini (70) katika mchezo tajwa hapo juu, kinyume na Kanuni ya 17.2(2.5) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 240: Namungo FC 2-1 Mtibwa Sugar Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kutokutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.



