Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said, ameweka wazi msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, akisema maandalizi yako katika hatua za mwisho na ujenzi utaanza hivi karibuni.
Hersi alisema moja ya ahadi kubwa iliyosalia kwa uongozi wake ni kuhakikisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Yanga katika eneo la Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam, unaanza rasmi na hatimaye kukamilika kwa wakati.
Kauli hiyo aliitoa jana, Julai 4, 2026, wakati wa sherehe za kuadhimisha ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ambao Yanga imeutwaa kwa mara ya tano mfululizo, katika hafla iliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya mamia ya wanachama na mashabiki, Hersi alisema uongozi umejipanga kuhakikisha ndoto ya uwanja wa kisasa inatimia, akisisitiza kuwa mchakato wa utekelezaji umefikia hatua muhimu ya mwisho.
โParedi la msimu ujao tutakalofanya tutatafuta sehemu nyingine na si hapa tena Jangwani, kwa sababu mwakani ujenzi wa uwanja utakuwa unaendelea katika kipindi hicho,โ alisema Hersi.
Alieleza kuwa hatua muhimu iliyobaki ni kukamilisha mchakato wa kubadili mfumo wa umiliki wa ardhi waliyopewa na Serikali, kutoka umiliki wa wanachama kwenda kwenye kampuni maalumu itakayosimamia utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa miundombinu.
Kwa mujibu wa Hersi, mabadiliko hayo yataisaidia klabu kuimarisha usimamizi wa uwekezaji na kuhakikisha mradi wa uwanja unatekelezwa kwa ufanisi na kwa viwango vya kisasa vinavyolenga kukuza hadhi ya Yanga ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumzia pia mipango ya kikosi, Hersi alikiri kuwa msimu uliopita ulileta changamoto kadhaa kutokana na baadhi ya wachezaji kushindwa kutoa mchango uliotarajiwa, licha ya usajili uliofanyika.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa katika dirisha hili la usajili, klabu itafanya maboresho makubwa ili kuhakikisha Yanga inarejea kwa nguvu mpya na kuendelea kutawala soka la Tanzania pamoja na kushindana kwa ufanisi kwenye michuano ya kimataifa.
Naye mfadhili wa klabu, GSM Group, aliendelea kutoa hamasa kwa mashabiki, akisisitiza kuwa Yanga itaendelea kubaki kileleni kwa kusema: โYanga Bingwa, mwakani tenaโฆโ alipozungumza kwa njia ya simu wakati wa sherehe za ubingwa zilizojaa shamrashamra Jangwani.
Mradi wa uwanja wa Yanga unaendelea kuwa miongoni mwa miradi mikubwa na inayosubiriwa kwa hamu na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, ukitarajiwa kubadilisha kabisa taswira ya miundombinu ya soka la Tanzania endapo utatekelezwa kama ilivyopangwa.



