Eneo la Jangwani, Dar es Salaam jijini Dar es Salaam liligeuka kuwa jukwaa la burudani na shamrashamra kubwa baada ya Simba SC kufanya maandamano ya kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, katika tukio lililovuta hisia za maelfu ya mashabiki waliomiminika kushuhudia historia hiyo.
Msafara wa mabingwa hao uliwasili eneo hilo majira ya saa 8:40 mchana, ukiwa umeongozwa na mabasi ya timu pamoja na msururu mkubwa wa mashabiki waliokuwa wamefurika barabarani, wakisubiri kuipokea timu yao baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye fainali iliyochezwa kisiwani Pemba.
Mara baada ya msafara huo kuingia Jangwani, ambako ndipo makao ya wapinzani wao wa jadi Yanga SC yalipo, mabasi ya Simba yalitembea kwa mwendo wa taratibu huku mashabiki wakiyazunguka wakishangilia kwa nguvu, wakiimba nyimbo za timu yao na kurusha vijembe vya ushindani wa jadi vilivyozidi kupamba tukio hilo.
Katika mandhari iliyochochea zaidi hisia za mashabiki, baadhi ya wapenzi wa Simba walionekana wakifuta vioo vya mabasi yao kama ishara ya furaha na mapenzi kwa klabu yao, huku wengine wakilielekezea vijembe basi la Yanga lililokuwa limeegeshwa pembeni ya eneo hilo, jambo lililoongeza joto la ushindani wa muda mrefu kati ya timu hizo mbili kubwa nchini.
Baadaye, gari la viongozi lililombeba msemaji wa klabu Ahmed Ally pamoja na nahodha Shomary Kapombe liliwasili likiwa limefunguka juu, likipokelewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki waliokuwa wamefurika.
Kapombe alionekana akilishika Kombe la CRDB na kulinyanyua mara kadhaa kuonesha furaha ya ushindi huo mbele ya mashabiki, huku Ahmed Ally akionyesha pia Kombe la Muungano ambalo Simba ilitwaa Aprili 2026 baada ya kuifunga Yanga, hatua iliyoongeza joto la sherehe hizo na kuongeza ladha ya ushindani.
Katika kile kilichoonekana kuongeza msisimko zaidi, viongozi hao walitumia muda kusimama mbele ya makao ya Yanga, wakinyanyua makombe yao huku mashabiki wakishangilia kwa nguvu na kuendelea kuimba nyimbo za klabu yao bila kuchoka.
Baadaye, Ahmed Ally alichukua kipaza sauti na kuwasalimia mashabiki, akitumia nafasi hiyo pia kutupia maneno ya utani kwa wapinzani wao, hali iliyochochea zaidi hamasa na shamrashamra katika eneo hilo lililokuwa limefurika watu na kelele za ushindi.
Ikumbukwe Yanga ilifanya poredi jana kusherehekea ubingwa wao wa tano mfululizo ligi kuu ya Tanzania Bara ambapo nao waliweka kambi ya muda mfupi mtaa wa Msimbazi yalipo Makao Makuu ya Simba wakiendeleza utani wa jadi.
Simba na Yanga ndio timu kongwe zaidi nchini na zimekuwa na upinzani wa kihistoria na haishangazi kuona zote zikianya paredi kubwa baada ya kutwaa mataji msimu huu.




