Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza rasmi ratiba ya usajili wa timu na wachezaji pamoja na kalenda ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) na Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) kwa msimu wa 2026/27. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, dirisha la kwanza la usajili lilianza Juni 25 na litafungwa Julai 25, 2026, likihusisha timu zitakazoshiriki hatua za awali za mashindano.
CAF imeeleza kuwa dirisha la pili la usajili litafunguliwa kuanzia Agosti 16 hadi Septemba 30, 2026 kwa ajili ya wachezaji watakaoshiriki hatua ya pili ya awali. Aidha, usajili wa hatua ya makundi utafanyika kati ya Oktoba 1 na Oktoba 31, 2026, huku dirisha la mwisho likifunguliwa Januari 2027 kabla ya kuanza kwa hatua za mtoano.
Kwa upande wa ratiba ya michezo, duru ya kwanza ya awali itachezwa kati ya Septemba 4 na 13, 2026, huku duru ya pili ikifanyika Oktoba 16 hadi 25. Hatua ya makundi imepangwa kuanza Novemba 27, 2026 na kumalizika Januari 24, 2027, kabla ya robo fainali kuchezwa Februari na Machi, nusu fainali Aprili, na fainali za mashindano yote mawili kufanyika kati ya Mei 9 na 31, 2027.
Mbali na kutangaza ratiba hiyo, CAF imethibitisha kuwa zawadi za fedha zitaendelea kubaki zilezile, ambapo bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika atazawadiwa dola za Marekani milioni 6, huku bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akipokea dola milioni 4. Aidha, kila klabu itaruhusiwa kusajili hadi wachezaji 40 kwa msimu, huku wachezaji tisa wakiruhusiwa kuwa kwenye benchi la wachezaji wakati wa mechi.