Klabu ya Young Africans (Yanga) ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kumsajili beki wa kushoto wa Mouna FC ya Ivory Coast, Samba Koné, kuelekea msimu mpya wa mashindano. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 anatajwa kuwa miongoni mwa malengo makuu ya Yanga katika kuimarisha safu ya ulinzi.
Kwa mujibu wa taarifa, Koné anatarajiwa kumaliza mkataba wake na Mouna FC mwezi huu, hali inayompa nafasi ya kujiunga na Yanga kama mchezaji huru bila ada ya usajili. Aidha, imeelezwa kuwa mazungumzo ya masharti binafsi yanaendelea vizuri, huku mchezaji huyo akionesha nia ya kuichezea klabu hiyo ya Jangwani.
Koné aliwahi kucheza kwa mkopo katika klabu ya Paradou AC ya Algeria kabla ya kurejea Mouna FC, ambako ameendelea kuonyesha kiwango kizuri. Msimu uliopita alitoa pasi nne za mabao na kujizolea sifa kama mmoja wa mabeki wa kushoto waliokuwa na kiwango bora katika Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Iwapo mazungumzo hayo yatakamilika kwa mafanikio, Koné anatarajiwa kuwa mbadala wa Boka katika nafasi ya beki wa kushoto na kuongeza ushindani ndani ya kikosi cha Yanga, huku klabu hiyo ikiendelea kujiimarisha kwa ajili ya mashindano ya ndani na yale ya kimataifa msimu ujao.