Klabu ya Yanga imemtangaza raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi, kuwa kocha mkuu mpya kuelekea maandalizi ya msimu wa 2026/27.
Mngqithi anatua Jangwani akiwa na uzoefu mkubwa wa kufundisha katika soka la Afrika, baada ya kufanya kazi kwa miaka kadhaa ndani ya klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Akiwa huko, alihudumu katika nafasi mbalimbali zikiwemo kocha msaidizi, kocha mwenza na kocha mkuu, akichangia mafanikio ya timu hiyo katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini na mashindano mengine ya ndani.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Mngqithi alikuwa akiifundisha Golden Arrows, pia ya Afrika Kusini, kufuatia kuondoka kwake Mamelodi Sundowns mwishoni mwa mwaka 2024.
Uteuzi wake unakuja wakati Yanga ikiendelea kujipanga kwa ajili ya msimu mpya, ikilenga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mngqithi anafahamika kwa falsafa ya soka inayosisitiza umiliki wa mpira, mashambulizi yenye mpangilio na nidhamu ya kiulinzi. Pia amejizolea sifa kwa uwezo wake wa kukuza vipaji vya wachezaji na kujenga timu zenye ushindani wa muda mrefu.