Safari ya kiungo wa kimataifa wa Congo Brazzaville, Innocent Loemba, ndani ya Simba SC inaelekea kufikia mwisho baada ya taarifa kueleza kuwa klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kuachana naye.
Loemba anatajwa kutokuwa sehemu ya mipango ya kocha mkuu Steve Barker kuelekea msimu mpya, huku benchi la ufundi likiwa kwenye mchakato wa kusafisha na kuunda upya kikosi chenye kuendana na falsafa ya kocha huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Barker hajamuweka Loemba kwenye mpango wake wa muda mrefu, jambo linaloifanya nafasi ya kiungo huyo kuendelea kubaki Msimbazi kuwa ngumu zaidi.
Loemba alitua Simba katika dirisha dogo la usajili akiwa na matarajio makubwa kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali za kiungo. Mwanzo wake ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ulikuwa wa kuvutia, akionyesha uwezo wa kumiliki mpira, kupiga pasi na kusaidia timu kwenye maeneo ya ushambuliaji.
Hata hivyo, kadri msimu ulivyoendelea, Loemba alianza kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo ndani ya timu pamoja na mabadiliko ya mipango ya benchi la ufundi.
Ujio wa Makgalwa Waongeza Ushindani
Moja ya mambo yanayotajwa kuchangia maamuzi ya Simba ni ujio wa winga Keletso Makgalwa kutoka Sekhukhune United, ambaye anatarajiwa kuongeza nguvu na ushindani katika eneo la pembeni na nafasi za ushambuliaji.
Simba imekuwa ikifanya maboresho kadhaa kwenye kikosi chake kuelekea msimu mpya, huku kocha Barker akitaka kuwa na wachezaji wanaoendana na mfumo na mahitaji yake ya kiufundi.