Winga wa Al Hilal ya Sudan, Jean Giramugisha, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda kwa msimu wa 2025-26 katika hafla ya utoaji wa tuzo iliyofanyika usiku wa jana. Nyota huyo alitunukiwa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora msimu mzima, akijidhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa zaidi katika ligi hiyo.
Kiwango hicho kimezifanya klabu kadhaa kuanza kumwania, huku Yanga SC ikitajwa kuwa miongoni mwa vinara wa mbio za kumsajili. Mbali na mabingwa hao wa Tanzania, Giramugisha pia anaripotiwa kufuatiliwa na klabu kutoka mataifa mbalimbali nje ya Afrika, ikiwemo Sporting Lisbon ya Ureno, ambazo zinavutiwa na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali za ushambuliaji, kasi yake na ubunifu wake mbele ya lango.
Giramugisha kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Al Hilal, hali inayomruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote. Hata hivyo, nyota huyo anatarajiwa kuitumikia Al Hilal katika michuano ya CECAFA Kagame Cup kabla ya kufanya uamuzi kuhusu hatma ya maisha yake yasoka.