Klabu ya Al Hilal imepoteza rasmi ubingwa wa Ligi Kuu ya Sudan msimu wa 2025/26 baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka la Sudan (SFA) kuidhinisha rufaa iliyowasilishwa na wapinzani wao wakubwa, Al Merrikh.
Uamuzi huo umebadili kabisa msimamo wa ligi, ambapo Al Hilal wameondolewa kileleni na kushushwa hadi pointi 18, huku Al Merrikh wakifikisha pointi 21 na kutawazwa mabingwa wapya wa Sudan.
Chanzo cha adhabu hiyo ni matumizi ya Al Hilal ya wachezaji wanane wa kigeni katika mechi dhidi ya Al Merrikh, idadi ambayo ilidaiwa kukiuka kanuni za mashindano. Baada ya kupitia rufaa ya Al Merrikh, Kamati ya Rufaa iliamua kuipa Al Hilal adhabu ya kupoteza mchezo kwa mabao 2-0, hatua iliyobadilisha msimamo wa mwisho wa ligi na kuondoa ubingwa mikononi mwao.
Uamuzi huo umeibua mjadala mkubwa ndani ya soka la Sudan, hasa kutokana na ukubwa wa ushindani kati ya Al Hilal na Al Merrikh, ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakitawala soka la nchi hiyo. Mara nyingi, ubingwa wa Sudan umekuwa ukiamuliwa kati ya vigogo hao wawili.
Al Hilal walikuwa wameonyesha kiwango bora uwanjani msimu huu, huku pia wakifanya vizuri katika michuano ya CAF Champions League. Hata hivyo, makosa ya kiutawala kuhusu usajili na matumizi ya wachezaji wa kigeni yamefuta mafanikio yao ya uwanjani na kuwagharimu taji la ligi.
Hata hivyo Al Hilal wamekatia rufaa uamuzi huo wakidai wachezaji watatu wanaolalamikiwa walipata uraia wa Sudan kihalali.