Mabingwa watetezi wa Kombe la CECAFA Kagame Cup, Singida Black Stars, wanatarajiwa kuingia kambini kesho Jumatano, Julai 15, 2026, kuanza rasmi maandalizi ya msimu wa 2026/27. Uamuzi huo unakuja wakati klabu hiyo ikijiandaa kutetea taji la Kagame Cup pamoja na kushiriki mashindano ya ndani msimu ujao.
Singida Black Stars wanaingia kambini wakiwa mabingwa watetezi wa Kagame Cup baada ya kutwaa ubingwa huo msimu uliopita kwa kuifunga Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Dar es Salaam. Mwaka huu, mashindano hayo yatafanyika Kigali, Rwanda kuanzia Julai 24 hadi Agosti 7, 2026.
Katika droo ya mashindano hayo, Singida Black Stars wamepangwa Kundi B pamoja na Simba SC, Jamus SC ya Sudan Kusini na Mogadishu City Club ya Somalia. Kundi hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya mtoano.
Mbali na kutetea ubingwa wa Kagame Cup, kambi hiyo pia ni sehemu ya maandalizi ya Singida Black Stars kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Uongozi wa klabu unaamini kuanza maandalizi mapema kutakipa kikosi muda wa kutosha kujenga ushindani na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana kwenye mashindano ya ndani na kimataifa.