Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kushirikiana na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, wametangaza mpira maalumu utakaotumika kuanzia hatua ya nusu fainali hadi mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia 2026.
Mpira huo unaoitwa Trionda Final ni toleo maalumu la mpira wa Trionda uliotumika katika hatua za makundi hadi robo fainali za mashindano hayo. Kwa mujibu wa Adidas, mpira huo umeendelea kubeba teknolojia na muundo wa awali, lakini umeongezewa muonekano mpya unaoendana na ukubwa wa mechi za hatua za mwisho za Kombe la Dunia.
Muundo wa Trionda Final umepewa heshima kwa kuenzi miji itakayokuwa mwenyeji wa hatua za mwisho za michuano hiyo ambayo ni Dallas, Atlanta, Miami na New York/New Jersey.
Mpira huo una mchanganyiko wa rangi za dhahabu, nyeupe na nyeusi, ambapo rangi ya dhahabu inaashiria thamani na hadhi ya Kombe la Dunia la FIFA, huku nyeusi ikiupa muonekano wa kipekee kuelekea mechi za kuwania ubingwa wa dunia.