Klabu ya Simba SC imezidi kuonyesha ubabe katika soko la usajili baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji tegemeo wa Sekhukhune United ya Afrika Kusini, Keletso Makgalwa (29), kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Taarifa za ndani kutoka ndani ya Msimbazi zinathibitisha kuwa miamba hiyo ya soka nchini imefikia muafaka wa mwisho na klabu ya Sekhukhune United pamoja na mchezaji huyo mwenyewe, huku masuala yote ya kimkataba na maslahi binafsi yakiwa yamekamilika kwa asilimia mia moja.
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker anatajwa ushawishi wake kufanikisha usajili wa winga huyo ambaye tetesi zinaeleza kuwa alikuwa akiwaniwa na watani zao Yanga ambao kocha wao mpya Manqoba Mngqith ambaye ni raia wa Afrika Kusini alitajwa kufanya mawasiliano na winga huyo kumshawishi bila ya mafanikio
Barker anajua vyema uwezo wa Makgalwa kwani amewahi kufanya naye kazi huko nyuma, ndiye aliyependekeza jina la nyota huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya winga wa kushoto na kiungo mshambuliaji wa kati.
Makgalwa amewahi pia kukipiga katika miamba ya soka ya Mamelodi Sundowns, anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi za mwisho, na uzoefu wa michuano mikubwa ya ndani na nje ya Afrika Kusini sifa ambazo benchi la ufundi la Simba linaamini zitakuwa msaada mkubwa katika kurejesha heshima ya klabu hiyo kitaifa na kimataifa.
Uongozi wa Simba SC unatarajiwa kumtambulisha rasmi nyota huyo hivi karibuni, huku kukiwa na matumaini makubwa kuwa usajili huu utaongeza nguvu kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi.