Klabu ya Simba SC imefanikiwa kuongeza muda wa huduma ya mshambuliaji wake Suleiman Mwalimu Gomez baada ya kufikia makubaliano mapya na klabu ya Wydad AC ya Morocco kuhusu mkataba wa mkopo wa msimu mzima.
Kwa mujibu wa taarifa, Mwalimu ataendelea kuvaa jezi ya Simba katika msimu wa 2026/27, huku klabu hiyo ikiendelea kunufaika na uwezo wake wa kufunga mabao na kusaidia safu ya ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo ameamua kusalia Msimbazi baada ya kuonyesha kiwango bora katika msimu wake wa kwanza, licha ya kuwepo kwa tetesi zilizomuhusisha na kuwindwa na wapinzani wa ndani zikiwemo Azam FC na Yanga SC.
Mwalimu alijiunga na Simba msimu uliopita kwa mkopo akitokea Wydad AC, na haraka akawa sehemu muhimu ya mipango ya benchi la ufundi kutokana na uwezo wake wa kumalizia mashambulizi.
Katika msimu uliopita, Mwalimu alikuwa mfungaji bora wa Simba kwenye mashindano yote, akifanikiwa kufunga mabao 15, rekodi iliyowafanya mabosi wa Simba warudi tena Morocco kwa waajiri wake Wydad kurefusha mkataba wake wa mkopo.