Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezikabidhi zawadi za fedha kwa timu za taifa za vijana kufuatia mafanikio yao makubwa katika mashindano ya kimataifa.
Serengeti Boys wamekabidhiwa Shilingi milioni 500 baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye Fainali za Kombe la Dunia la FIFA zitakazofanyika nchini Qatar, sambamba na kutinga fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) nchini Morocco.
Kwa upande wa Tanzanite Queens, wamepokea Shilingi milioni 50 ikiwa ni pongezi kwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 17, zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu nchini Poland.
TFF imeeleza kuwa zawadi hizo ni kutambua juhudi, uzalendo na mafanikio ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hizo, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka la vijana nchini.